Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yazindua tovuti mpya ya miongozo kuhusu mlo

Picha:FAO

FAO yazindua tovuti mpya ya miongozo kuhusu mlo

Shirika la Kilimo na Chakula, FAO limezindua tovuti mpya ya miongozo kuhusu mlo, ambayo itakuwa kama jukwaa la kubadilishana taarifa kuhusu mienendo bora ya lishe kote duniani.

Tayari, tovuti hiyo imeanza kukusanya miongozo ya lishe kutoka zaidi ya nchi 100, na itaendelea kuongezewa maelezo pale miongozo mipya inapoandaliwa na kusahihishwa.

Miongozo kuhusu mlo katika chakula ina lengo la kuweka msingi wa mlo, lishe, afya, sera za kilimo na mipango ya elimu kuhusu lishe, ili kuendeleza mienendo bora ya ulaji na hali ya maisha yenye afya.

Miongozo hiyo inalenga kutumia ujumbe mfupi unaotokana na taaluma ya kisayansi kuhusu ulaji wenye afya na maamuzi kuhusu mienendo ya maisha ya afya, ili kutoa maelezo kwa umma kuhusu ni vyakula gani na mienendo ipi ya ulaji itakayowapa lishe wanayohitaji katika kuimarisha afya na kuzuia magonjwa sugu.