Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake ni nguzo muhimu dhidi ya utapiamlo: ICN2

Wanawake ni nguzo muhimu dhidi ya utapiamlo: ICN2

Wanawake ni nguzo muhimu katika kuchagiza harakati dhidi ya utapiamlo, na huo ni ujumbe wa Muungano wa jamii ya watu wa asili wanaohamahama mwishoni mwa mkutano wa pili wa kimataifa wa lishe mjini Roma, Italia.

Akizungumza kwa niaba ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, wakati wa sherehe ya kuhitimisha mkutano huo Munkhbolor  Gungaa kutoka Muungano huo amesema mkutano huo ungalizingatia zaidi ushahidi uliopo wa jukumu la wanawake katika kuboeresha  lishe na afya.

(SAUTI Munkhbolor)

“Utambuzi wa kina wa haki za binadamu za wanawake ni muhimu katika kufanikisha haki ya chakula na lishe kwa watu wote. Na kwa mantiki hiyo tunatoa wito kwa nchi wanachama kutunga sera za  kuwawezesha wanawake kuwa na likizo ya uzazi ya malipo, msaada wakati wa kunyonyesha mtoto sehemu za kazi, na ulinzi wote wa kijamii”.

Halikadhalika, Bi Gungaa amesema mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yalitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha jamii inatambua kazi zinazofanyika bila malipo, kuongeza usawa katika mgao wa majukumu ya kazi majumbani kati ya wanaume na wanawake wa majukumu ya kaya.

Aidha ametowa wito kwa serikali kuhakikisha  aina zote za ukatili dhidi ya wanawake zinatokomezwa.