Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya vifo vya Ebola Mali yaongezeka, WHO yachukua hatua

Kituo cha tiba cha Ebola katika Kenema, Sierra Leone. Picha: UN Picha / Ari Gaitanis

Idadi ya vifo vya Ebola Mali yaongezeka, WHO yachukua hatua

Kisa kingine cha Ebola kimebainika huko Mali na hivyo kufanya idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo nchini Mali kuongezeka na kufikia Sita, huku shirika la afya duniani WHO likitangaza hatua za kudhibiti kuenea kwa Ebola. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

WHO imesema idadi hiyo ya vifo Sita nchini Mali ni pamoja na mtoto wa miaka miwili aliyeingia na ugonjwa huo nchini humo na kufariki dunia tarehe 24 mwezi uliopita.

Mtoto huyo hakuambukiza mtu yeyote aliyekutana naye lakini kirusi kiliingizwa tena Mali na mwanaume aliyetokea Guinea na alifariki dunia tarehe 27 mwezi uliopita.

Visa vyote vipya vina uhusiano kwa njia moja au nyingine na mgonjwa aliyetibiwa kwenye kliniki ya Pasteur mjini Bamako.

Wakati huo huo WHO imechukua hatua kuzuia kuenea kwa Ebola kwa kuhakkisha mataifa 14 ya Afrika yaliyo hatarini zaidi kupata Ebola yanatekeleza mpango wa WHO wa hatua kumi za kudhibiti Ebola. Fadelah Chaib ni msemaji wa WHO Geneva.

(Sauti ya Fadelah)

“Hadi sasa WHO imeunda jopo  na wadau kwenda kwenye nchi hizo 14, ni muhimu sana mathalani kujiuliza je tuna uwezo wa kuchukua hatua haraka na kushirikisha jamii, kujikinga,kuwa na ufuatiliaji wa mlipuko, maabara na ufuatiliaji wa watu ambao mgonjwa amekutana nao? Kwa hiyo ni sehemu ya mambo kumi ya viashiria ambavyo hizo nchi 14 zitapatiwa.”