Ahadi zilizotolewa kwa GCF ni ishara njema kwa mabadiliko ya tabianchi:Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha ahadi za serikali za kutoa dola Bilioni Tisa nukta Tatu kama mtaji wa mfumo wa miradi endelevu isiyoharibu mazingira, GCF.
Ahadi hizo zimetolewa wakati wa mkutano wa ahadi uliofanyika huko Berlin, Ujerumani.
Ban amekaririwa na msemaji wake akieleza kuwa ahadi hizo ni kiashiria kuwa serikali zinazidi kuelewa manufaa yatokanayo na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na madhara yanayoweza kupatikana iwapo hatua zitachelewa kuchukuliwa.
Amesema uchangiaji wa fedha kwa miradi ya kiuchumi isiyoharibu mazingira ni hatua bora katika kuelekea kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu mabadiliko ya tabianchi mwakani huko Paris.
Katibu Mkuu ameziomba nchi zote zilizoendelea ambazo hazijatoa ahadi zao kwenye mfuko huo GCF, ziwe zimefanya hivyo kabla ya kuanza kwa mkutano wa 20 wa mabadiliko ya tabianchi COP20 utakaoanza huko Lima Peru tarehe Mosi mwezi ujao.