Harakati dhidi ya ugaidi, Kenya yatangaza hatua ilizochukua:Balozi Muli

19 Novemba 2014

Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi  Koki Muli Grignon amesema uanzishwaji wa miradi yenye lengo la kutokomeza umaskini ni mojawapo ya hatua za serikali za kukabiliana na vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali.

Akihutubia Baraza hilo wakati wa mjadala wa ngazi ya juu wa wazi kuhusu ugaidi, wapiganaji mamluki Balozi Muli amesema miradi hiyo inatekelezwa kupitia mamlaka za majimbo nchini Kenya kupitia mfumo wa ugatuaji madaraka.

Amesema ugatuaji wa matumizi ya fedha na uchukuaji wa maamuzi kwenye maeneo  husika ni msingi wa kutokomeza umaskini na tayari hatua hiyo ya  ugatuaji imejumuishwa kwenye katiba ya Kenya.

Hata hivyo pamoja na hatua hizo Balozi Muli amesema wanaunga mkono harakati a Umoja wa Mataifa dhidi ya ugaidi..

(Sauti ya Balozi Muli)

“Na nyongeza ya hapo tunakaribisha jitihada za sasa za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Benki ya dunia na wadau wa maendeleo kwenye dira yao ya kuweka mazingira ya Amani endelevu kwenye ukanda huu kupitia miradi bora ya uendelezaji miundombinu kwa mashauriano na Muungano wa Afrika, miradi ambayo itafungua eneo hilo kwa biashara na uwekezaji. Serikali ya Kenya pia imeridhia misingi minne ya mkakati wa kimataifa dhidi ya ugaidi.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter