Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yakamilisha ziara ya ukaguzi Zimbabwe

Picha: IAEA

IAEA yakamilisha ziara ya ukaguzi Zimbabwe

Maofisa waandamizi ambao ni wataalamu masuala ya nyuklia na uzuiaji wa mionzi leo wamekamilisha ziara ya siku kumi nchini Zimbabwe iliyokuwa na lengo la kukagua namna nchi hiyo inavyozingatia mwongozo uliotolewa na Shirika la Nguvu la Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA kwa nchi kuzingatia usalama wa mionzi na masuala mengine. Taarifa kamili na George Njogopa.

(Taarifa ya George)

Timu hiyo ya wataalamu yenye jukumu la kupitia masuala mbalimbali imemaliza ziara hiyo na kisha kutoa mapendekezo kwa serikali ya Zimbabwe na chombo chake cha mamlaka ya mionzi kuongeza ufanisi ili kuliwezesha taifa hilo kufikia viwango vinavyotolewa na Shirika la nguvu za atomiki duniani.

Patricia Holahan kutoka Marekani ndiye aliyeongoza ujumbe huo wa wataalamu waliotoka katika nchi za Ubelgiji, Hungary, Namibia, Nigeria na Sweden. Msafara huo pia ulikuwa na wataalamu wengine watatu kutoka shirika hilo la atomiki.

Akizungumzia kuhusua hatua zilizopigwa na Zimbabwe, Holahan alisema kuwa licha ya kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake lakini mamlaka ya mionzi ya Zimbabwe imefanikiwa kupiga hatua kubwa kimaendeleo.