Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola yakwamisha harakati dhidi ya HIV/AIDS Afrika Magharibi:UNAIDS

Mfanyakazi wa WHO akifuatilia na kubaini watu ambao wamewasiliana na mtu mwenye ugonjwa wa Ebola. Picha: WHO/C. Black/Sierra Leone

Ebola yakwamisha harakati dhidi ya HIV/AIDS Afrika Magharibi:UNAIDS

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloongoza mapambano dhidi ya Ukimwi, UNAIDS limesema sasa ni dhahiri shahiri kuwa mlipuko wa Ebola unafuta mafanikio yaliyopatikana awali dhidi ya Ukimwi.

Naibu Mkurugenzi wa UNAIDS Luiz Loures amesema hayo alipozungumza katika mahojiano maalum na Eleutério Guevane wa Radio ya Umoja wa Mataifa baada ya ziara yake kwenye nchi za Afrika Magharibi zilizokumbwa na Ebola.

Ametolea mfano Sierra Leone ambayo hadi sasa imekumbwa na vifo Elfu Moja vya Ebola, akisema kuwa mafanikio makubwa iliyopata dhidi ya Ukimwi sasa yanatokomea kwani hata huduma za kujikinga na Ukimwi zimekumbwa na mkwamo.

(Sauti ya Luiz)

“Tuna ushahidi mathalani kwenye kupata huduma dhidi ya Ukimwi, tuna pungufu ya asilimia 30 ikilinganishwa na kiwango cha kabla ya mlipuko wa Ebola. Asilimia Tisa ya wajawazito waliokuwa wanapatiwa huduma ya kuzuia maambukizi ya kirusi cha Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hawapati huduma hizo hivi sasa.”