Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa vyoo ni hatari kwa kila mtu: UNICEF

UN Photo/Patricia Esteve
UN Photo/Patricia Esteve

Ukosefu wa vyoo ni hatari kwa kila mtu: UNICEF

Wakati wa kuadhimisha Siku ya Vyoo Duniani Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF limeonya kwamba maendeleo ya pole pole kuhusu kujisafi na mazoea yaliyojikita ya kujisaidia katika maeneo ya wazi kati ya mamilioni ya watu kote duniani yanaendelea kuwaweka watoto na jamii zao hatarini.

Katika taarifa, UNICEF imesema karibu watu bilioni 2.5 kote duniani hawana vyoo vya kutosha na kati yao bilioni 1 hujisaidia haja kubwa katika eneo lililo wazi, mathalan katika mashamba, misitu, au vyanzo vya maji na hivyo kuwaweka hususan watoto katika hatari ya kuambukizwa magonjwa kama kuhara.

Huko Tanzania Zanzibar harakati nazo zinaendelea za kuhakikisha kuna vyoo kama anavyosema Rukia Mohammed, Afisa afya, Wizara ya afya visiwani  humo.

(SAUTI RUKIA)

Mwaka wa 2013, zaidi ya watoto 340,000 walio chini ya miaka mitano walikufa kutokana na magonjwa ya kuhara yanayotokana na ukosefu wa maji safi na salama, mazingira safi na usafi wa msingi, hali ambayo kwa wastani husababisha vifo 1,000 kwa siku.

Mkuu wa maji na kujisafi kimataifa wa shirika la UNICEF , Sanjay Wijesekera, amesema ukosefu wa mazingira safi ni alama ya kuaminika ya hali halisi ya watu masikini katika nchi. Wijisekera amesema japo idadi kubwa ya watu masikini hawana vyoo, kila mtu anaathiriwa na madhara ya kujisaidia katika maeneo ya wazi, hivyo kila mmoja anapaswa kushughulikia tatizo hili.