Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakosoaji nusura walinishawishi kukata tamaa- mshindi wa tuzo ya Sayari Dunia

Taka la plastiki. (Picha ya UNEP(Video capture)

Wakosoaji nusura walinishawishi kukata tamaa- mshindi wa tuzo ya Sayari Dunia

Mwanaharakati wa mazingira ambaye ameshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya ‘Bingwa wa Sayari Dunia’ kufuatia mpango wake wa kusafisha bahari amesema mara kwa mara alitaka kukata tamaa kwa sababu alikumbana na kukosolewa mno.

Boyan Slat, ambaye alisitisha masomo yake ya chuo kikuu kwa muda ili akabiliane na tatizo la kuondoa taka za plastiki baharini, amewaambia waandishi wa habari kuwa wataalam wa viwanda walisisitiza kuwa hilo lilikuwa haliwezekani. Mamia ya kampuni alizoomba kumpa ufadhili zote zilikataa, ila moja tu.

Nilihisi ni kama wanasema, ‘hatutaki kuona hili likifanyika.’ Ilikwenda kinyume na kile tumeambiwa miaka kumi iliyopita, kwamba bahari haiwezi kusafishwa. Na sasa kwa sababu nimesema kuna njia ya kusafisha, hilo linatatanisha hadithi yao, na kushawishi vitendo vyao pia, na kwangu mimi wakati huo ulikuwa mgumu mno.”

Slat amesema, taka nyingi za plastiki hupatikana karibu ufukoni. Kwa sasa, boti hutumiwa kukusanya taka kwa kutumia vyandarua, lakini vyandarua hivyo hunasa samaki na viumbe wengine baharini pia.

Wazo la Slat, raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 20, ni kuweka kuzuizi kinachoelea majini upana wa kilomita 100, na ambacho kitakusanya taka za plastiki na kuziweka mahali pamoja ili zioondolewe na kutumiwa tena.

Mradi wake wa OceanCleanup sasa umepokea dola milioni 2 kutoka kwa wafadhili kwenye intaneti.