Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti yafichua nuru ya ufugaji samaki, mlo wa vichwa na mifupa yake yapigiwa chepuo

Mfugaji wa samaki akilisha samaki katika moja ya bwawa analofugia samaki hao huko Nhan My, Vietnam. (Picha: FAO)

Ripoti yafichua nuru ya ufugaji samaki, mlo wa vichwa na mifupa yake yapigiwa chepuo

Ufugaji wa samaki katika muongo mmoja ujao, unatarajiwa kuongezeka kuliko ilivyotarajiwa na hivyo kutoa fursa ya kuboresha lishe miongoni mwa mamilioni ya watu hususan Afrika na barani Asia.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolea na Shirika la chakula na kilimo duniani FAO ikipigia chepuo kuongezwa kwa uwekezaji katika sekta hiyo kutokana na kuongezeka kwa biashara ya samaki duniani.

Uwekezaji unaochagizwa ni ule wa teknolojia ya matumizi ya maji, utotoaji wa samaki na virutubisho vya mlo wa samaki hao ili kuongeza uzalishaji kwa zaidi ya asilimia Nne ifikapo mwaka 2022.

Mtaalamu wa samaki na lishe kutoka FAO Jogier Toppe amesema samaki wana virutubisho muhimu na hivyo ufugaji wao utaboresha pia lishe ya jamii.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya kaya zenye vipato vikubwa hukimbilia kula minofu ya samaki ilhali virutubisho kama vile madini ya chuma, Calcium na zinki hupatikana kwenye kichwa cha samaki na mifupa ambavyo mara nyingi hutupwa.

FAO imetoa wito kwa serikali kutunga sera zitakazorahisisha operesheni za ufugaji wa samaki ambao licha ya kuongeza kipato cha kaya hurutibisha lishe.