Kipindi cha mpito cha kiraia Burkina Faso kianze haraka iwezekanavyo: Ibn Chambas
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Afrika Magharibi, Dkt. Mohammed Ibn Chambas amesema mazungumzo ya kurejesha utulivu nchini Burkina Faso yanaendelea vyema kati ya vyama vya siasa, vikundi vya kiraia na wananchi upande mmoja na viongozi wa kijeshi.
Akihojiwa na Derrick Mbatha wa Radio ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Chambas amesema hadi sasa kila upande unaonyesha mwelekeo wa kulegeza msimamo wake kwa lengo la hatimaye kuwa na utawala wa kiraia.
Hata hivyo amesema mazungumzo yanapaswa kuzaa matunda mapema iwezekanavyo kwani tayari vikao kadhaa vya ngazi ya juu vimeshafanyika ikiwemo vile vya wakuu wa jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.
(Sauti ya Ibn Chambas)
“Ni jambo la dharura kwa kipindi hicho cha mpito kuanza, naweza kusema kuwa ndani ya siku moja au mbili, hiki kipindi cha mpito kianze kikiongozwa na raia ambaye atachaguliwa kuwa Rais na ambaye ataongoza mchakato wa mpito na kuanza kushughulikia kufanyika kwa uchaguzi huru na haki ili wananchi wa Burkina Faso kwa mara nyingine wawe na fursa ya kuchagua kiongozi wao.”
Mwishoni mwa mwezi uliopita Rais Blaise Compaoré ambaye ameongeza Burkina Faso kwa miaka 27 alitangaza kujiuzulu baada ya maelfu ya waandamanaji kuandamana kwenye mji mkuu Ouagadougou wakikabiliana na vikosi vya usalama .