Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya muundo wa Baraza la Usalama iko mikononi mwenu:Kutesa

UN Photo/Devra Berkowitz
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Sam Kutesa,(

Hatma ya muundo wa Baraza la Usalama iko mikononi mwenu:Kutesa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu uwiano wa uwakilishi kwenye Baraza la Usalama ambapo Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa amesema hatma ya marekebisho iko mikononi mwa nchi wanachama waUmoja huo.

Kutesa amesema safari ya kufanya marekebisho hayo imekuwa ni ndefu licha ya mwaka 2005 viongozi wa dunia kutaka baraza hilo liwe na uwakilishi wenye uwiano.

(Sauti ya Kutesa)

Mamlaka ya majadiliano yako mikononi mwenu nchi wanachama. Ni matumaini yangu kuwa mjadala wa leo utakuwa ni msingi thabiti wa marekebisho ya baadaye na kuchochea mijadala zaidi ya siku za usoni.”

Bwana Kutesa amesema ni vyema mjadala huo wa marekebisho ya uwakilishi kwenye Baraza la Usalama yakasongeshwa kwa pamoja kwa kuwa jitihada hizo si muhimu tu kwa kuimarisha utendaji wa chombo hicho bali pia kuendeleza uhalali wa uwepo wake.

Bara la Afrika katika mjadala huo liliwakilishwa na Mwakilishi wa kudumu wa Sierra Leone kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vandi Chidi Minah ambaye amesema kinachotakiwa siyo tu mjadala bali..

(Sauti ya Balozi Minah)

“Tunatoa wito kwa wote wale wanaotaka marekebisho ya Baraza la Usalama kuelekea katika mchakato wa dhati. Hoja yetu ni kwamba mashauriano ya dhati ndiyo yataleta marekebisho dhati.”

Baraza la Usalama tangu kuanzishwa kwake lina wajumbe 15 ambapo watano kati yao ni wa kudumu na wana kura turufu.

Wajumbe hao wa kudumu ni Ufaransa, Uingereza, Marekani, Urusi na China.