Heko Burkina Faso kwa maridhiano juu ya kipindi cha mpito:Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amepongeza wananchi wa Burkina Faso kwa kuridhia makubaliano ya kimsingi kuhusu mwaka mmoja wa kipindi cha mpito nchini humo kitakachoongozwa na raia kitakachowezesha uchaguzi wa kidemokrasia mwezi Novemba mwakani.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi ikiwa ni siku kadhaa baada ya Rais Blaise Compaore kujiuzulu na jeshi kutangaza kuchukua madaraka.
(Sauti ya Dujarric)
"Mjumbe wake maalum, Mohammed Ibn Chambas amekaribisha makubaliano hayo yaliyofikiwa jana Ouagadougou kati ya pande zote ili kusuluhisha kwa amani mzozo wa kisiasa Burkina Faso. Ametoa wito kwa pande zote kuendelea kushiriki kwenye mashauriano ya dhati kwa lengo la kuanzisha kipindi cha bayana cha mpito kwa maridhiano.”
Halikadhalika Katibu Mkuu ameunga mkono jitihada za pamoja za usuluhishi za Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika na jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS pamoja na marais wa Ghana, Nigeria, na Senegal bila kusahau wadai wa kimataifa zenye lengo la kuhakikisha kipindi cha mpito Burkina Faso kinakuwa cha amani.