Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha zaidi zahitajika kukidhi mahitaji ya mlipuko wa Ebola- OCHA

Mhudumu wa afya akivalia sare ya kujikinga wakati wa kuwahudumia waathiriwa wa ugonjwa wa Ebola,Kailahun,Sierra Leone.Picha:IRIN/Tommy Trenchard

Fedha zaidi zahitajika kukidhi mahitaji ya mlipuko wa Ebola- OCHA

Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, imesema kuwa fedha zaidi zinahitajika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya mlipuko wa Ebola, kwani kufikia sasa ni dola milioni 572 ndizo zilizopatikana, ikiwa ni asilimia 58 tu  ya jumla ya dola milioni 988 zilizoombwa.

Mfuko wa pamoja wa wadau wa kukabiliana na Ebola umepokea dola milioni 60.6, kutokana na ahadi zilizotolewa za hadi dola milioni 119.

Nchini Sierra Leone, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na dharura ya Ebola, UNMEER unashirikiana na kituo cha kitaifa cha kukabiliana na Ebola ili kuwafikishia wahudumu wote wa kitaifa malipo yao ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi kabla ya mwisho wa mwezi, kwani wengi wao hawana akaunti za benki na hivyo ni vigumu kuwalipa.

Kwingineko, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP linanunua na kusafirisha hadi Sierra Leone magari 74 kutoka Benki ya Dunia, yakiwa ni pamoja na magari aina ya ambulance na yale ya kubeba maiti.