IFC yapiga chepuo sekta binafsi Guinea, Liberia na Sierra Leone kutokana na Ebola

5 Novemba 2014

Shirika la Kimataifa juu ya Usimamizi wa Fedha, IFC ambalo ni miongoni mwa taasisi za Kundi la Benki Kuu ya Dunia imetangaza fungu la dola Milioni 450 kwa ajili ya kuwezesha biashara, uwekezaji na ajira huko Guinea, Liberia na Sierra Leone, nchi ambazo zimekumbwa zaidi na Ebola.

Taarifa ya IFC imesema mpango huo wa kuchagiza sekta binafsi unahusisha dola Milioni 200 zitawekezwa kwenye miradi ya haraka zaidi na kiasi kilichobakia kitaelekezwa kwenye miradi ya kujikwamua kiuchumi kutokana na Ebola.

Fedha zitapatiwa benki Sita zenye ushirika na IFC kwenye nchi hizo ambapo kampuni binafsi zinaweza kupatiwa kwa ajili ya miradi kama vile uagizi wa bidhaa za msingi ikiwem nishati, chakula na kilimo.

Rais wa benki ya dunia Jim Yong Kim amesema Ebola ni janga la kibinadamu lakini linaathiri pia uchumi wa Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Amesema IFC itaangalia jinsi ya kuinua biashara na uwekezaji kwenye eneo hilo la Afrika Magharibi ili kuhakikisha sekta binafsi inaendeleza majukumu yake na ikiwemo utoaji wa ajira katika mazingira magumu ya sasa

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud