Ukatili wa makundi yaliyojihami kwa misingi ya kikabila na kidini ni changamoto: Kamishna Zeid

4 Novemba 2014

Kamishana wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Husssein amesema wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya miaka thelathini ya kupitishwa kwa Mkataba dhidi ya Mateso na Ukatili kwamba, mkataba huo ni chombo muhimu cha sheria ya kimataifa, lakini licha ya maendeleo ya kila siku, katika kila bara, wanawake, wanaume na watoto wanateswa kwa makusudi na mawakala wa serikali.

Katika taarifa, Kamishna Mkuu Zeid amesisitiza changamoto za kuendelea kuutekeleza mkataba huo, zikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi na ukatili dhidi ya makundi ya kikabila na kidini unaotekelezwa na makundi yaliyojihami yasiyokuwa ya kiserikali na hali mbaya mno ya haki za binadamu za wahamiaji.

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema kuwa mateso yanayoendelea kote duniani yanaathiri pakubwa watu binafsi na jamii, akisisitiza jukumu muhimu la mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na ya kiraia katika kutimiza malengo ya mkataba dhidi ya mateso.

Aidha, Ban amesema, nchi zinapaswa kuchukua hatua mathubuti za kutokomeza mateso na kurejesha waathirika katika hali yao ya awali.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter