Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yatoa dola milioni 3.5 kusaidia operesheni za kibinadamu Nigeria

Nembo ya OCHA

OCHA yatoa dola milioni 3.5 kusaidia operesheni za kibinadamu Nigeria

Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, imetenga dola milioni 3.5 kutoka kwa mfuko wa huduma za dharura, CERF kwa ajili ya kusaidia operesheni zakibinadamu kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa hivi karibuni na shirika la kitaifa la kudhibiti masuala ya dharura, zaidi ya watu 740,000 wamelazimika kuhama kufuatia mapigano kati ya kundi la Boko Haram na jeshi la serikali tangu Januari mwaka uliopita.

OCHA imesema wengi wa waathiriwa wamekimbilia kwa jamii za wenyeji ambapo wanaendelea kukabiliana na hali mbaya ya afya na kujisafi, na kwa mujibu wa mratibu wake mkazi nchini Nigeria, Daouda Toure, fedha za CERF zitatumiwa kusaidia katika ulinzi, pamoja na huduma za afya, maji na kujisafi katika majimbo ya Yobe na Borno.