Hali ya usalama Kivu Kaskazini bado inatia wasiwasi- OCHA

4 Novemba 2014

Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, imesema kuwa mashambulizi yanayotekelezwa na makundi yaliyojihami huko Beni katika jimbo la Kivu ya Kaskazini, yamewaua watu wapatao 100 tangu mapema mwezi Oktoba na kuwalazimu takriban 20,000 wengine katika eneo hilo kuhama makwao.  OCHA imesema watu 14 wengine wameuawa katika siku chache zilizopita.

Mashirika ya kibinadamu yametoa wito wa kuwalinda raia na wahudumu wa kibinadamu kuweza kufanya kazi yao bila vizuizi.

Mashirika ya kibinadamu Kivu Kaskazini yameanza kutoa misaada kwa familia zilizoathiriwa, na pia kutoa huduma za afya na matibabu. Kivu Kaskazini ndilo jimbo lenye hali tete zaidi, likiwa na makundi mengi yenye silaha. Kufikia sasa, watu wapatao 861,000 wamekimbia makwao ndani ya jimbo hilo, ikiwa ni thuluthi moja ya idadi nzima ya wakimbizi wa ndani milioni 2.7 katika DRC.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter