Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya habari duniani yaunganisha nguvu kukabili ebola

Elimu kwa umma kupitia redio kuhusu ebola nchini Cote D'voire.(Picha ya UNICEF ya video)

Mashirika ya habari duniani yaunganisha nguvu kukabili ebola

Mashirika ya kimataifa ikiwamo lile la mwasiliano duniani ITU pamoja na chama cha Internet ISOC leo kwa pamoja yametangaza mkakati wao wa kuunganisha nguvu ili kukabiliana na homa ya ebola. Taarifa kamili na George Njogopa.(Taarifa ya George)

Katika mkutano wao wa pamoja uliofanyika katika mji wa kitalii duniani wa Busan huko Korea Kusini mashirika hayo ambayo yanaheshimika duniani kwa teknolojia ya mawasiliano yamesema kuwa yanajitupa kwenye vita hivyo kwa vile yanatambua jukumu lake katika kupambana na balaa hilo.

Yamesema wakati dunia ikiendelea kuhangaika na kitisho cha ugonjwa wa ebola, kuna umihimu pia wa kuhakikisha kwamba sekta ya upashaji habari inachukua jukumu kubwa katika vita hivyo kwa kutumia mbinu mbalimbali za utoaji habari.

Yamesema kuwa utoaji habari kwa wakati, usambazaji wa huduma muhimu za mawasiliano kama vile simu za mkononi na kuwepo kirahisi kwa huduma za internet kutasaidia kwa kiwango kikubwa kuwaweka wananchi katika hali ya tahadhari na kuwaandaa kadri inavyopaswa.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa pamoja, Katibu Mkuu Mtendaji wa ITU Dr Hamadoun I. Touré alisema kuwa ili kukabiliana na homa hiyo ambayo imeziathiri zaidi nchi za Afrika magharibi, hakuna njia nyingine ya mkato mbali ya kutumia kila kinachowezekana ikiwamo teknolojia hiyo ya mawasiliano.