Baraza la Usalama lalaani vitendo vya ISIL Iraq

UN Photo.
Baraza la Usalama.

Baraza la Usalama lalaani vitendo vya ISIL Iraq

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani utekaji nyara na mauwaji ya  jamii ya Wasunni yaliyotekelezwa na wanamgambo wanaotaka kuweka dola la Uislamu wenye msimamo mkali, ISIL katika mkoa wa Anbar nchini Iraq.

Miili ya waliouawa ilipatikana katika makaburi ya halaiki.

Wengi wa wale waliouawa wamekuwa wakipambana na ugaidi kwa kushirikiana na Serikali ya Iraq.

Baraza la Usalama limesema, uhalifu huu kama mauwaji yaliyofanyika  katika kambi ya Speicher mjini Tikrit, kwa mara nyingine tena unaonyesha ukatili wa ISIL, na ni dhihirisho bayana kwamba makundi ya kigaidi nchini Iraq yanalenga makundi na madhehebu yoyote ya wakazi wa Iraq.

Katika taarifa, wanachama wa Baraza la Usalama wameelezea masikitiko yao kuhusu wananchi wa Iraq waliouawa na raia kutoka mataifa mengine  waliouawa, kubakwa au kuteswa na ISIL, sawa na kusajiliwa na kutumiwa kwa watoto kwa ajili ya vita.

Halikadhalika wanachama wa Baraza hilo walisistiza haja ya wale waliokiuka sheria ya kibinadamu ya kimataifa nchini Iraq kuwajibishwa, wakibaini kwamba baadhi ya vitendo hivi vinaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Aidha, Baraza la Usalama pia limetoa wito kwa serikali ya Iraq na  jumuiya ya kimataifa, kuhakikisha kuwa watekelezaji wa uhalifu watachukuliwa hatua za kisheria.