Vita, mizozo na majanga vyatishia MDGs Afrika:Ripoti

1 Novemba 2014

Ripoti mpya iliyozinduliwa  Jumamosi kwenye warsha ya kiuchumi barani Afrika huko Addis Ababa Ethiopia imesema wakati idadi ya Waafrika wanaofurahia viwango vya juu maishani ikiongezeka, nchi za Afrika zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara ni lazima ziongeza juhudi zao za kuhakikisha mizozo ya kisiasa, majanga na magonjwa kama vile Ebola huko Afrika Magharibi haziathiri mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana.

Kwa mujibu wa Ripoti hiyo viwango vya umaskini barani Afrika vimeendelea kushuka, licha ya ongezeko la hivi karibuni la bei za vyakula na mafuta na kudorora kwa uchumi wa dunia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ya tathmini ya malengo ya maendeleo ya milenia, MDG, Mkurugenzi wa UNDP barani Afrika, Abdoulaye Machi Dieye amesema, changamoto ni kuhakikisha Afrika, ikisaidiwa na washirika wa kimataifa inaendelea kuwekeza katika sekta zitakazobadili  maisha ya watu wa kawaida.

Amesema iwapo Afrika inataka kusonga mbele inachohitaji ni uchumi mahiri, watu wenye afya na elimu, jamii thabiti na isambaze huduma bora za mitaa.

Kuhusu Ebola, ripoti hiyo itolewayo kila mwaka na Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB, Tume ya Uchumi ya Afrika, ECA, Tume ya Umoja wa Afrika, UAC na UNDP imesema ugonjwa huo unatishia maendeleo yaliyopatikana ikiwemo kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kuelekea ukomo wa MDG mwaka 2015.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter