Serikali ridhieni mkataba wa kudhibiti matumizi ya Zebaki: Mtaalam

31 Oktoba 2014

Mtaalamu mpya maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na sumu, Baskut Tuncak ametoa wito kwa serikali ambazo hazijaridhia mkataba wa kimataifa wa Minamata kuhusu athari za matumizi ya Zebaki kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.

Tuncak ametoa ombi hilo kabla ya mkutano muhimu wa kamati ya kiserikali ya mazungumzo juu ya Zebaki, utakaofanyika Bangkok, Thailand kuanzia tarehe Tatu hadi Saba mwezi Novemba.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imemkariri Tuncak akisema kuwa kisheria mkataba wa Minamata ni lazima uridhiwe na nchi 50, lakini tangu ufunguliwe mwezi Oktoba 2013 kwa ajili ya kutiwa saini ni nchi saba tu ndizo zimeridhia kati ya 128 zilizosaini.

Amesema kwa kasi ya sasa mkataba huo hautaweza kuanza kutumika ifikapo mwaka 2020 kama ilivyokubaliwa.

Mtaalamu huyo ambaye amechukua jukumu hiyo hivi karibuni amesema ni jambo jema serikali kuzingatiwa wajibu wao wa haki za binadamu akisema kuwa kuchelewa kuridhia ni sawa na kusema binadamu na mazingira yataendelea madhara ya uchafuzi utokanao na matumizi ya zebaki.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter