Ripoti ya ICC inatia wasiwasi kuhusu utendaji kazi wa mahakama hiyo- Balozi Macharia Kamau

31 Oktoba 2014

Mwakilishi wa Kenya wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, Macharia Kamau, amesema kuwa inatia huzuni na kuvunja moyo kuona kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC imeweza kutoa hukumu moja tu na kuwakilisha waathiriwa 8,040 katika kesi sita pekee, katika miaka kumi ya uwepo wake, kulingana na ripoti mahakama hiyo ya hivi karibuni.Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa Grace)

Balozi Kamau ameyasema hayo jana jioni katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo lilikutana kujadili kuhusu ripoti ya kumi ya shughuli za ICC.

“Katika ulimwengu ambao umeghubikwa na machafuko na vita vya uharibifu na ambapo mamia ya maelfu au hata mamilioni ya watu wamefariki dunia katika miaka kumi iliyopita, inashangaza kuwa ICC ina hukumu moja tu ya kujivunia kwa kazi yake, na idadi ndogo ya waathiriwa 8,040 pekee. ICC imejiripoti kuwa na upungufu mkubwa kwa nchi wanachama.”

Akirejelea yaliyomo katika ripoti hiyo ya ICC, Balozi Kamau amesema haishangazi kuwa kwa mara ya kwanza kabisa, hakuna nchi mpya mwanachama iliyoridhia mkataba wa Roma katika kipindi cha mwaka mmoja inaomulika ripoti hiyo, kwani Mahakama hiyo imeshindwa kuzishawishi nchi kwa kazi yake.

“Kwa sisi ambao tumeshirikiana na mahakama hii katika miaka michache iliyopita, ni dhahiri kuwa hatua za dharura ni lazima zichukuliwe iwapo mahakama hii inataka kudumu kama taasisi ya kimataifa inayoaminika. Kenya inasikitishwa na ufahamu na utekelezaji wa sasa wa Mkataba wa Roma, na kwetu sisi, huenda hili ndilo linaloidhoofisha mahakama hii.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter