Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na kuibuka upya kwa uhasama huko Sudan Kusini

Watoa huduma wa afya UNMISS. Picha ya UM

Ban asikitishwa na kuibuka upya kwa uhasama huko Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani vikali kuanza tena kwa uhasama kati ya jeshi la serikali la Sudan Kusini, SPLA na vikikundi kinzani vilivyojihami vya Bentiu na Rukbona kwenye jimbo la Unity.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akisema kuwa kitendo hicho kwa mara nyingine tena ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha uhasama na yanatishia jitihada za IGAD za kusaka suluhu la kudumu la kisiasa kwenye mzozo wa Sudan Kusini.

Ametoa wito kwa Rais Salva Kiir na Riek Machar kusitisha mara moja operesheni za kijeshi huku akiwakumbusha wajibu wao wa kulinda raia na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.

Halikadhalika Katibu mkuu amekumbusha pande zote kutokiuka kanuni dhidi ya maeneo ya Umoja wa Mataifa ikiwemo vituo vya hifadhi vya raia ambako ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini umepatia makazi zaidi ya wakimbizi 100,000 wa ndani.

Kati yao hao, 49,000 wako mjini Bentiu.

Ban pia amesihi pande zote kushiriki kwa dhati kwenye mashauriano yanayoendelea Addis Ababa Ethiopia na hatimaye kufikia makubaliano ya mamlaka jumuishi za mpito.