Ban na Kenyatta washuhudia kuanzishwa mkakati endelevu wa usafiri Afrika.

30 Oktoba 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wameshuhudia kupitishwa kwa mkakati wa kihistoria ambao utachagiza mfumo mpito wa usafiri, utakaokuwa na manufaa kwa afya, mazingira na maendeleo endelevu barani Afrika.Mkutano huo kuhusu Mfumo endelevu wa Usafiri Afrika uliandaliwa na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, UNEP, Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Makazi UN-Habitat.

Katibu Mkuu amepongeza serikali za Afrika kwa kuchukua hatua ya kuunda mkakati endelevu wa usafiri, akiongeza kuwa ahadi ya kuendeleza na kudumisha miundombinu ya kuaminika, ya kisasa, endelevu na nafuu katika maeneo ya mijini na vijijini inaoana vyema na Ajenda 2063 ya Maendeleo.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta amesema, mkutano huu unakuja wakati Afrika ikiwa mbioni kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka 50, Ajenda 2063.

Ukuaji kasi wa miji nchini Kenya unatarajiwa kuongeza idadi ya magari maradufu katika kipindi cha miaka sita, hali ambayo itahatarisha afya na maisha ya maelfu ya watu, kwani matumizi ya mafuta ya petroli yanaongeza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Kimataifa, uchafuzi wa hewa unakadiriwa kuwaua watu milioni 7 kila mwaka,  hii ikiwa ni mara nne zaidi ya vifo vitoakanavyo na Ukimwi na malaria kwa pamoja.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter