Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya Ebola vyatimu 4,920; WHO yasema maambukizi huenda yanapungua

Picha: WHO

Vifo vya Ebola vyatimu 4,920; WHO yasema maambukizi huenda yanapungua

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoratibu shughuli za kukabiliana na Ebola, UNMEER, umetoa ripoti mpya ya hali ya mkurupuko wa Ebola kufikia leo Oktoba 30, ikionyesha kuwa watu 4,920 walikuwa wamefariki dunia kufikia tarehe 27 Oktoba, huku visa vya maambukizi vikiwa vimefikia 13,703.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa kumeshuhudiwa kupungua kwa viwango vya maambukizi, lakini likionya kuwa ni mapema mno kufanya hitimisho kutokana na viashiria hivyo.

Mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power, amekamilisha ziara yake Afrika Magharibi, baada ya kukutana na Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa UNMEER, Anthony Banbury, mjini Accra, Ghana.

Bi Power ameema serikali ya Marekani imejitoa kupambana na Ebola, akisifu UNMEER kama silaha muhimu ya kuzuia kirusi cha Ebola kusambaa kutoka maeneo kilipoanzia, na baadaye kuwaambia waandishi habari:

Kuna haja ya ahadi zaidi na haja ya kutimiza ahadi zaidi, ili kubadili hali. Kuna haja ya vitanda zaidi, haja ya fedha zaidi ili kuwalipa wachagizaji wa kijamii na watu wanaofanya mazishi salama, na kwa kufanya hivyo, tutawalinda sio tu watu katika nchi zilizoathiriwa, lakini pia watu katika nchi zetu zenyewe.”