Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel isitishe mpango wa makazi mapya Yerusalem Mashariki: Ban

Jeffrey Feltman akihutubia Baraza la usalama. (Picha: UN/Eskinder Debebe)

Israel isitishe mpango wa makazi mapya Yerusalem Mashariki: Ban

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mkutano kuhusu Mashariki ya Kati likijikita zaidi kwenye suala la mustakhbali wa Palestina.Mkuu wa masuala ya siasa kwenye umoja huo Jeffrey Feltman alihutubia akisema kuwa Katibu Mkuu anatiwa wasiwasi na ripoti mpya za ujenzi wa makazi mapya Elfu Moja ya walowezi kwenye eneo la Yerusalem Mashariki linalokaliwa na Israeli.

Ameliambia baraza kuwa taarifa hizo mpya zinafuatia uamuzi wa Israeli wa mwishoni mwa mwezi uliopita wa kuharakisha mchakato wake wa ujenzi wa makazi 2,600 huko Givat Hamatos, Yerusalemu Mashariki.

(Sauti ya Feltman)

“Iwapo zitatekelezwa, mipango hii kwa mara nyingine tena itaibua tashwishwi juu ya azma ya Israel ya kufikia Amani ya kudumu na wapalestina kwa kuwa makazi hayo mapya yanatishia uwezekano wa kuwa na taifa la Palestina.”

Feltman amemkariri Katibu Mkuu Ban akiisihi Israel kubadili uamuzi huo na badala yake iitikie wito wa jamii ya kimataifa wa kuzingatia sharia za kimataifa na mpango uliokubaliwa kupitia mchakato wa amani.

Amesema huu ni wakati wa kudhihirisha uongozi wa kijasiri kwa pande zote kujizatiti kwenye mashauriano ya dhati ili hatimaye taifa la Israel na lile Palestina yaweze kuwepo kwa pamoja.