UNAMID ilificha baadhi ya matukio, Ban achukizwa

29 Oktoba 2014

Jopo lililochunguza madai ya kuficha taarifa kwa makusudi dhidi ya ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, Sudan, UNAMID limebaini kuwepo walakini kwenye utoaji taarifa za matukio ya eneo hilo.

Jopo liliundwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kufuatia madai kuwa UNAMID ilikuwa inaficha kwa makusudi baadhi ya matukio ya uhalifu dhidi ya raia au walinda Amani.

Jopo lilichunguza matukio 16 yanayodaiwa ripoti zake za kina kufichwa kwa makusudi ambapo lilishindwa kupata ushahidi wa kuficha kwa makusudi lakini ilibainika kuwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa hayakupatiwa ripoti kamili juu ya mazingira ya vitendo hivyo.

Halikadhalika imebainika kuwa UNAMID iliendelea kuwa kimya wakati ingaliweza kuandaa taarifa kwa vyombo vya habari hata kama hakukuwepo na ukweli kuhusu matukio hayo.

Stephan Dujarric ni msemaji wa Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu mkuu amechukizwa sana na matokeo haya. Anatambua kuwa UNAMID inakabiliwa na changamoto za kipekee kwenye utekelezaji wa majukumu yake kulingana na mazingira inayofanya kazi. Hata hivyo kuwa kimya na kutoa taarifa kiduchu kwa matukio yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na vitisho au mashambulio dhdi ya walinda Amani wa Umoja wa Mataifa hakuwezi kukubalika katika mazingira yoyote.”

Amesema Katibu Mkuu atachukua hatua zozote za lazima ili kuhakikisha utoaji wa taarifa kutoka UNAMID unakuwa sahihi na kwa wakati.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter