Sudan Kusini, UN wazindua kampeni ya kupinga kuwasili watoto jeshini

29 Oktoba 2014

Serikali ya Sudan Kusini kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa leo imezindua kampeni maalumu yenye lengo la kuwaepusha watoto kutotumika kama askari.Kampeni hiyo yenye kauli mbiu ‘hawa ni watoto na wala siyo askari’ inadhihirisha namna taifa hilo lilivyodhamiria kutokomeza vitendo vya utumikishaji watoto katika uwanja wa mapambano. Taarifa kamili na George Njogopa.

(Taarifa ya George)

Uzinduzi wa kampeni hiyo umewajumuisha maofisa kadhaa wa serikali ya Sudan Kusini na wale wa Umoja wa Mataifa ambao wote wamekubaliana kuendelea kushirikiana ili kuleta tija kwa watoto.

Walioshiriki kwenye uzinduzi huo ni pamoja Mwakilishi wa Katibu Mkuu anayehusika na watoto walioko kwenye maeneo yenye vita Bi Leila Zerrougui na maofisi wengine kutoka UNICEF.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalohusika na Watoto UNICEF limekuwa likichukua jukumu kubwa kuipiga jeki Sudan Kusini ili kukomesha utumikishaji watoto kwenye mizozo kwa kuweka mkakati maalumu ambao unasisitiza kuwa ifikapo mwaka 2016 hakuna watoto tena wanaingizwa jeshini.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini Kuol Manyang Juuk alisema kuwa serikali imedhamiria kuona kwamba suala la utumikishaji watoto linakuwa historia.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter