Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atua Somalia na Kenya kwenye ziara yake Pembe ya Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwa nchini Somalia na Rais wake Hassan Sheikh Mohamud.(Picha ya UM/Ilyas Ahmed

Ban atua Somalia na Kenya kwenye ziara yake Pembe ya Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, aliyeko ziarani eneo la Pembe ya Afrika, leo amezuru Somalia na kukutana na rais wake, kabla ya kuelekea Kenya ambako atakuwa na shughuli kadhaa. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Akiwa Somalia, Ban ambaye ameandamana na Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, na viongozi wengine, amesema  kuwa wanajua changamoto za kisiasa, utawala, usalama na maendeleo ni kubwa mno, lakini wamejitoa kuisaidia Somalia kukabiliana nazo.

Ameongeza kuwa wana mani kuwa Somalia inaweza kuimarisha maendeleo iliyopiga kufikia sasa, kwani sasa kuna misingi mingi ya kuwezesha hilo, kwani kuna ishara nyingi za kutia matumaini.

Akizungumza kuhusu Al-Shabab, Bwana Ban amesema kuwa ingawa nguvu za kundi hilo zimedidimia, bado halijaondolewa. Amepongeza jeshi la serikali ya Somalia na AMISOM kwa mchango wao kwa amani na utulivu Somalia. Baada ya Somalia, viongozi hao wametua nchini Kenya, ambako Katibu Mkuu atakutana na Rais Uhuru Kenyatta na pia kuzindua kampeni ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji.