Safari ya kudhibiti Ebola bado ni ndefu lakini kuna mabadiliko: Balozi Power

28 Oktoba 2014

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power aliyeko ziarani Liberia kujionea hali halisi ya mlipuko wa Ebola amesema bado safari ni ndefu kutokomeza ugonjwa huo lakini mwelekeo uko sahihi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu Liberia baada ya kutembelea maeneo kadhaa ikiwemo vituo vya matibabu amesema mipango iliyowekwa ni sahihi na kinachohitajika hivi sasa ni utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na ugonjwa huo.  Ametolea mfano ujenzi wa maabara ya uchunguzi dhidi ya Ebola.

 (Sauti ya Balozi Power)

 "Leo tumetembelea kitongoji cha Bong ambako kuna maabara ya uchunguzi wa Ebola inayohama kutoka eneo moja hadi jingine, ambapo kabla ya kuwepo maabara hiyo ilichukua siku tano kwa sampuli kutoka Bong  kwenda Monrovia kwa uchunguzi na ndipo upate majibu. Lakini sasa hivi siyo tena siku tano bali chini ya saa Tano.Hii inawezesha watu wasio na Ebola kuruhusiwa kutoka vituo vya tiba na kutoa fursa kwa wengine.”

Waandishi wa habari walimuuliza Balozi Power iwapo atakaporejea nyumbani atatekeleza karantiki iliyowekwa na baadhi ya majimbo nchini Marekani kwa wasafiri kutoka Afrika Magharibi ikiwemo wahudumu wa Afya.

(Sauti ya Balozi Power)

“Nitaheshimu sheria na masharti yoyote yaliyowekwa. Baadhi ya mazingira nchini Marekani yanabadilika mara kwa mara, na serikali kuu inawasiliana na majimbo ambako kunawasili watu wanaorejea kutoka ukanda huu. Halikadhalika tutaendelea kufuatilia taarifa kuhusu masharti yanayopaswa kuzingatiwa kadri zinapopatikana.”

Akizungumza kwenye mkutano huo Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia ameshukuru mshikamano kutoka kwa wadau akisema inatia moyo kwenye harakati dhidi ya Ebola.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter