Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuepuke kujenga hofu wakati tunadhibiti kuenea kwa Ebola: Ban

UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu Ban Ki-moon (kulia) akihutubia mkutano wa Mawaziri wa Nje wa Mamlaka ya Serikali za Kimataifa kuhusu Maendeleo (IGAD) mjini Addis Ababa, Ethiopia. Pia pichani: Nkosazana Dlamini Zuma (katikati), Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, na Carlos Lopes, Katibu Mtendaji wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika.Picha:

Tuepuke kujenga hofu wakati tunadhibiti kuenea kwa Ebola: Ban

Ukubwa wa janga la Ebola usiwe chanzo cha kujenga hofu na badala yake hatua stahili zinapaswa kuchukuliwa kwa umakini, ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyotoa wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Ban amesema kasi ya kuenea kwa Ebola ni kubwa kuliko uwezo wa kudhibiti lakini hiyo isiwe sababu ya kujenga hofu miongoni mwa watu kwani hatua za kukabiliana nazo zinafahamika.

Mathalani ametolea mfano uamuzi wa baadhi ya nchi kuweka karantini dhidi ya wahudumu wa afya na hata mipakani akisema hilo litakwamisha jitihada dhidi ya Ebola.

Badala yake Katibu Mkuu amesema kinachotakiwa sasa ni kuimarisha jitihada za kimataifa kukabiliana na ugonjwa huo kwa pamoja kwani hakuna nchi au ukanda ambao unaweza kudhibiti Ebola peke yake.

Ban ambaye kwenye mkutano huo alifuatana na Rais wa benki ya dunia, Jim Yong Kim na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma amesifu ushiriki wa utatu wa taasisi hizo, yaani Umoja wa Mataifa, benki ya dunia na Muungano wa Afrika dhidi ya Ebola.

Ameshukuru nchi zilizojitolea kwa hali na mali kusaidia kudhibiti kuenea zaidi kwa Ebola huko Guinea, Liberia na Sierra Leone.