Watoto milioni 2.6 zaidi walitumbukia katika umaskini wakati wa mdororo wa kiuchumi katika nchi tajiri- UNICEF

28 Oktoba 2014

Ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, inaonyesha kuwa  zaidi ya watoto milioni mbili na nusu katika nchi tajiri walitumbukia katika umaskini kufuatia mdororo wa uchumi.

Ripoti hiyo yenye kichwa, “Watoto wa mdororo: athari za mdororo wa kiuchumi kwa maslahi ya mtoto katika nchi tajiri”,  inaorodhesha nchi 41 za OECD na Muungano wa Ulaya, ikitumia vigezo vya ikiwa viwango vya umaskini wa watoto umeongezeka au umepungua tangu mwaka 2008. Inafuatilia pia viwango vya vijana kati ya umri wa miaka 15-24 ambao hawapo shuleni, hawana ajira au hawapati mafunzo. Yekaterina Chzhen ni mtaalam wa sera za jamii na uchumi katika UNICEF

"Tunakadiria kwamba watoto milioni 2.6 wametumbukia katika umaskini katika nchi tajiri zaidi duniani tangu mwaka 2008, na hivyo kufikisha milioni 76.5 idadi nzima ya watoto wanaoishi katika umaskini katika nchini zilizoendelea."

Ripoti inasema kuwa, ingawa mipango ya baadhi ya nchi ya kuchochea uwekezaji na matumizi iliweza kuwalinda watoto kutokana na umaskini, kufikia mwaka 2010, nchi nyingi ziliachana na kuchochea matumizi na kuanza kupunguza matumizi, na hivyo kuathiri maslahi ya watoto vibaya, hususan katika eneo la Mediterenia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter