Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifaa vya usaidizi dhidi ya Ebola vyawasili Mali

Dawa za kukabiliana na Ebola.Picha ya WHO/M. Missioneiro

Vifaa vya usaidizi dhidi ya Ebola vyawasili Mali

Ndege ya Umoja wa Mataifa ikiwa na shehena ya tani Moja ya vifaa tiba dhidi ya Ebola imewasili mwishoni mwa wiki kwenye mji mkuu wa Mali, Bamako ikiwa ni siku chache baada ya kuripotiwa kwa mgonjwa wa Ebola nchini humo.

Vifaa hivyo vya Shirika la afya duniani ni pamoja na vile vya kujikinga vinavyotumiwa na wahudumu wa afya kama vile barakoa, glovu pamoja na ndoo.

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP ambalo ndilo linaratibu safari za ndege za misaada ya dharura kutoka Umoja wa Mataifa limesema kasi ndiyo msingi wa kukabiliana na Ebola.

Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Magharibi Denise Brown amesema shehena ilisafirishwa kutoka Monrovia, Liberia ambako ndio kitovu cha usafirishaji wa vifaa hivyo.