Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huu ni wakati wa fursa kwa Pembe ya Afrika- Ban

Somalia ni moja ya nchi zitakazonufaika.Picha ya OCHA

Huu ni wakati wa fursa kwa Pembe ya Afrika- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye yuko ziarani nchi za Pembe ya Afrika, amesema kuwa Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na wadau wengine, wameungana katika azma yao ya kuzisaidia nchi za ukanda huo.

Akizungumza leo mjini Addis Ababa, Ethiopia, Ban amesema kuwa huu ni wakati wa fursa kubwa kwa ukanda wa Pembe ya Afrika, ambao unakabiliwa na changamoto nyingi, kuanzia ukame hadi ugaidi na dhana zenye misimamo mikali.

Katibu Mkuu amesema kuwa licha ya changamoto hizo, ukanda huo una nchi zenye uchumi unaokuwa haraka, huku maendeleo ya kuelekea ustawi wa kisiasa yakishuhudiwa.

Ban amesema sasa ndio wakati wa jamii ya kimataifa kuimarisha uungaji mkono wake kwa juhudi hizo za kikanda.

Katibu Mkuu pia amegusia suala la amani, akisema kuwa amani na maendeleo katika ukanda wa Pembe ya Afrika vinakwenda sambamba, kama ilivyo popote pale duniani.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa kikanda, umoja na mazungumzo ni muhimu katika kupatia suluhu migogoro na matatizo mengine ambayo hayana mipaka.