Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaojitolea kudhibiti Ebola wanapaswa kulindwa siyo kunyanyapaliwa: Ban

Mhudumu wa afya anazungumza na mama amekuwa katika mazingira ya watu waliokufa kutokana na Ebola nchini Sierra Leone.(Picha ya WHO/C.Black)

Wanaojitolea kudhibiti Ebola wanapaswa kulindwa siyo kunyanyapaliwa: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza wasiwasi wake juu ya vizuizi vilivyowekwa hivi karibuni dhidi ya watu waliotembelea nchi zilizokumbwa na ugonjwa wa Ebola.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amemkariri Ban akisema kuwa vizuizi hivyo vinaweka shinikizo zaidi kwa wahudumu wa afya ambao wamekuwa mstari wa mbele kukabiliana na Ebola.

(Sauti ya Dujarric)

“Wahudumu wa afya wanaorejea kutoka maeneo hayo ni watu wa kipekee waliojitolea kwa ajili ya ubinadamu. Hawapaswi kukumbwa na vizuizi visivyozingatia misingi ya kisayansi. Hao wanaopata maambukizi wanapaswa kusaidiwa badala ya kunyanyapaliwa.”

Msemaji huyo amemkariri Katibu mkuu akisisitiza kuwa njia pekee ya nchi kujikinga dhidi ya Ebola ni kusaidia kuepusha kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo huko Afrika Magharibi.

Amesema jambo hilo linahitaji kupelekwa wahudumu zaidi wa afya na kuwapatia msaada wanaporejea nyumbani kwani jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuwalinda.