Guinea inawatesa wafungwa- UN

27 Oktoba 2014

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imeelezea hali mbaya wanaokumbana nayo watu walioko vizuizini nchini Guinea ambako baadhi yao wamewekwa kwenye mlundikano mkubwa jambo linalotishia afya zao. Taarifa kamili na George Njogopa.

(Taarifa ya George)

Ripoti hiyo ambayo inafuatia ziara iliyofanywa na maofisa wa kutoka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imefichua hali halisi katika magereza mengi nchini humo. Ripoti hiyo imesema kuwa watu wengi wanaendelea kushikiliwa katika vituo kadhaa huku wengine wakinyanyaswa na hata kupuuzwa kwa haki zao za msingi.

Mathalani ripoti hiyo imefichua kile inachosema vitendo vya udhalilishaji pamoja na matukio ya unyanyasaji ambayo siyo tu kwamba yanakwenda kinyume na sheria za kimataifa bali pia yanakwenda kinyume na utu wa binadamu.

Maofisa wa haki za binadamu wamesema kuwa wakati walipotembelea magereza mbalimbali katika mji mkuu wa Conakry walibaini kuwepo kwa matukio mengi yanayokwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu ikiwamo kwa watuhumiwa wengine kuenda kusota gerezani pasipo kufikishwa mahakamani.

Ripoti hiyo imeitaka serikali kuongeza kasi ya utendaji ili kuona kwamba wale wanaoendelea kushikiliwa wanakuwa kwenye mazingira mazuri yanayokubalika kimataifa.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter