Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu za vipindi vya Radio na Televisheni ziko hatarini: UNESCO

UN Photo/Tobin Jones)
Picha za nyaraka za Radio Mogadishu. Picha:

Kumbukumbu za vipindi vya Radio na Televisheni ziko hatarini: UNESCO

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova amezungumzia umuhimu wa kuhifadhi nyaraka za picha na sauti kwa ajili ya vizazi vijayo.

Amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya urithi wa taarifa za picha na sauti Oktoba 27 akiongeza kuwa urithi huo unabeba mafunzo, taarifa na ufahamu ambao ni muhimu kuhamishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Bokova amesema urithi huo kama vile filamu, vipindi vya radio na televisheni una kumbukumbu za msingi za karne ya 20 na 21 na husaidia kuendeleza utambulisho wa kitamaduni wa kila jamii.

Hata hivyo amesema licha ya umuhimu huo, kumbukumbu lukuki zimepotea tangu kuibuka kwa teknolojia za sauti na picha ambazo zinawezesha watu kubadilishana picha na sauti kwa urahisi zaidi.

Amesema ni kwa mantiki hiyo mwaka 2005 iliamuliwa kuwepo kwa siku hii ya kimataifa ili hatua za makusudi zichukuliwe kuhifadhi nyaraka hizo kama sehemu ya kuendeleza utambulisho wa kitaifa.