Siku ya Umoja wa Mataifa: Ban ahimiza ushirikiano ili kufikia malengo ya pamoja

24 Oktoba 2014

Leo Oktoba 24 ni Siku ya Umoja wa Mataifa, na katika ujumbe wake kuadhimisha siku hii, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema kuwa Umoja huo unahitajika hata zaidi wakati huu ambapo kuna matatizo mengi.

Ban amesema matatizo ya umaskini, magonjwa, ugaidi, ubaguzi na mabadiliko ya tabianchi, yote yana athari mbaya mno kwa ulimwengu.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa mamilioni ya watu wanaendelea kudhulumiwa kupitia ajira za kulazimishwa, usafirishaji haramu wa wanadamu, utumwa wa ngono na kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama mashambani, viwandani na katika kuchimba migodi, huku uchumi wa kimataifa ukisalia kuwa usio na usawa.

Ban ameongeza kuwa malengo ya maendeleo ya millennia yameweka msukumo kwa kampeni iliyofana zaidi dhidi ya umaskini, na kutoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kurejelea ahadi yao ya kuwawezesha watu waliotengwa na walio wanyonge.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter