Kuelekea uchaguzi mkuu Burundi, kuna mwelekeo sahihi muhimu mshikamano

23 Oktoba 2014

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, Parfait Onanga-Anyanga amesema licha ya changamoto zilizopo kuelekea uchaguzi mkuu 2015 nchini Burundi, yapo mafanikio ambayo yanaweza kutumika kuweka msingi wa uchaguzi huru na wa haki.

Parfait Onanga-Anyanga, amesema hayo alipozungumza na Derrick Mbatha wa Radio ya Umoja wa Mataifa baada ya kikao cha tatu kilichofanyika Gitega nchini Burundi kutathmini utekelezaji wa mpango wa kuelekea uchaguzi huo.

Amesema kwa kuangalia historia ya Burundi ilikotoka na kile kinachoendelea sasa ikiwemo mfumowa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliotumika kwenye chaguzi mbili hiyo ni hatua kubwa lakini..

(Sauti ya Onanga-Anyanga)

“Bado tuna suala la kutokuvumiliana, kwani siyo wadau wote wanafahamu kuwa kila mtu ana haki ya kuzungumza au kila mtu ana haki ya kuwa na mtazamo tofauti na kwamba hilo halipaswi kusababisha misuguano.”

Kuhusu iwapo uchaguzi mkuu utakuwa huru na wa haki, Bwana Onanga-Anyanga amesema hilo linawezekana na kinachotakiwa sasa ni mshikamano kwani..

(Sauti ya Onanga-Anyanga)

Iwapo sote tutashiriki vyema, yaani serikali, vyama vya upinzani na usaidizi wa wadau tutaweza kufanikiwa. Ilikuwa hivyo mwaka 2005 na mwaka 2010 japo kulikuwepo na masuala kadhaa lakini naamini kwa ujumla hilo ni lengo ambalo tunaweza kufikia.”

Mkutano wa Gitega ulihudhuriwa na wadau kadhaa ikiwemo maafisa wa serikali, viongozi wa vyama vya upinzani, na wawakilishi wa vikundi vya kiraia.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter