Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za BRICS zashauriana kuhusu kupambana na utapiamlo kabla ya ICN2

Nchi tno zafanya mkutano kushauriana kuhusu utapiamlo.(Picha ya Fao)

Nchi za BRICS zashauriana kuhusu kupambana na utapiamlo kabla ya ICN2

Nchi tano wanachama wa kundi la BRICS, ambazo ni Brazil, Urusi, India, Uchina, na Afrika Kusini, zimefanya mkutano mjini Roma kushauriana kuhusu jinsi ya kupambana na utapiamlo, wakati maandalizi ya kongamano la pili la kimataifa kuhusu lishe, ICN2, ambalo litafanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Katika mkutano huo unaofanyika makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, wazungumzaji wamesisitiza kuwa tatizo la kutokuwa na usalama wa chakula na utapiamlo yanaweza kupatiwa suluhu tu kwa kuwa na utashi thabiti wa kisiasa, kuwekeza rasilmali za kutosha na kuhakikisha kuwa wizara husika na wadau wasio wa kiserikali wanashirikiana kwa uratibu mzuri.

Mkutano huo wa BRICS kuhusu lishe, ambao umeandaliwa ili kuongeza ufahamu na kuchagiza mjadala kuhusu masuala muhimu yanayohusu lishe, unafuatia makubaliano yaliyosainiwa siku chache zilizopita baina ya nchi wanachama wa FAO na Shirika la Afya Duniani, WHO kuhusu azimio na mkakati wa kuchukua hatua, yakiwemo mapendekezo 60 ya kisera ambayo yanalenga kuhakikisha kuwa watu duniani wanapata milo yenye afya zaidi.

Akiufungua mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi wa FAO na Mratibu wa Maendeleo ya Kijamii na Kicuhumi, Jomo Kwame Sundaram, ametaja aina tatu za utapiamlo, ambazo ni njaa ya mara kwa mara, utapiamlo wa ukosefu wa virutubishi katika chakula au njaa iliyojificha, na magonjwa yasiyoambukiza kama utipwatipwa, yanayohusishwa na mlo.