Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola bado ni tishio kwa afya ya umma: WHO

Mlipuko wa Ebola unakandamiza mafanikio ya uzazi salama.(Picha ya UNFPA Liberia/Calixte Hessou)

Ebola bado ni tishio kwa afya ya umma: WHO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la afya duniani , WHO dkt. Margaret Chan ameridhia mapendekezo ya kamati ya masuala ya dharura ya shirika hilo kuhusu ugonjwa wa Ebola yanayosema kuwa bado ugonjwa huo ni tishio kwa ya umma duniani. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kamati hiyo ilikutana Geneva, Uswisi na kuwasilisha mapendekezo hayo baada ya kutathmini hali ya halisi na kuona maambukizi yanaongezeka kwa kasi kubwa ikiwa hadi sasa kuna visa 9936 ambapo kati ya hivyo watu 4877 wamefariki dunia.

Kamati imetaka pia kuendelea na jitihada kudhibiti maambukizi mapya hususan kwenye nchi tatu zilizokumbwa zaidi ambazo ni Liberia, Sierra Leone na Guinea.

Dkt.  Isabelle Nuttall, ni Mkurugenzi wa WHO akihusika na hatua za dharura.

(Sauti ya Dkt. Nuttal )

“Uchunguzi wa ziada na wakina bado ni muhumu zaidi ili kupunguza kusafirisha ugonjwa wa Ebola kutoka nchi moja kwenda nyingine. Na hii inapaswa kufanyika kwa watu wote wanaoondoka viwanja vya ndege vya kimataifa, bandari, na hata mipaka mikubwa kwenye nchi hizo tatu.”

Hata hivyo kamati imerejelea msimamo wake kuwa hakuna sababu yoyote ya kuweka zuio la safari au biashara.