Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna hofu na ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya wahamiaji: Afrika

Wakimbizi kutoka Syria waokolewa katika bahari ya Mediterenia. Picha@UNCHR/A. d'Amato(UN News Centre)

Tuna hofu na ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya wahamiaji: Afrika

Bara la Afrika limeelezea hofu yake juu ya ongezeko la vitendo vya ubaguzi, unyanyasaji na hata kuenguliwa kwa wahamiaji kwenye maeneo mbali mbali duniani.

Akihutubia Kamati ya Tatu ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Janet Karim kutoka Malawi ambaye amezungumza kwa niaba ya Afrika ametaka kubadilika kwa mtazamo dhidi ya wahamiaji kwani inakandamiza haki zao.

Kwa mantiki hiyo amesema wanaunga mkono harakati za ofisi ya haki za binadamu za utetezi wa kubadilishwa kwa mwelekeo huo.

Halikadhalika Bi. Karim amesema Afrika inaamini kuwa hakuna ukanda wowote duniani unaweza kujivuna kuwa imekidhi haki za binadamu, bali ni jukumu la kila nchi kwenye eneo husika kuwa na utashi wa kisiasa na rasilimali ili kuhakikisha  haki hizo ikiwemo za kisiasa, kijamii na kiuchumi zinazingatiwa.