Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Libya suluhu ni ya kisiasa tu: UNSMIL

Nembo ya UNSMIL

Mzozo wa Libya suluhu ni ya kisiasa tu: UNSMIL

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Bernadino Leon amekuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa Libya Abdullah Al-Thini nchini Malta.

Katika mazungumzo hayo, Bwana Leon amempatia muhtasari waziri mkuu huyo juu ya mashauriano yaliyozinduliwa nchini Libya tarehe 29 mwezi u uliopita baina ya wabunge wa nchi hiyo, mashauriano ambayo yanawezeshwa na Umoja wa Mataifa

Leon ambaye ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa Libya, UNSMIL, amesisitiza kuwepo kwa azma baina ya pande zote zinazovutana ya kutaka kuhakikisha mashauriano hayo yanaleta maafikiano.

Amesema licha ya wasiwasi wake kuhusu ongezeko la mashambulizi ya kijeshi na wito wa hatua zaidi za aina hiyo ambao haukuweka mazingira mazuri wakati wa mashauriano, Bwana Leon amesema ni matumaini yake kuwa pande zote husika pamoja na wananchi wa Libya watawezesha kufikia suluhu siku za usoni.

Waziri Mkuu Al-Thini alielezea hofu yake kuhusu hali ngumu ya usalama na ya kibinadamu lakini wote wawili wamekubaliana kuwa jitihada zote lazima zilenge kusuluhisha mzozo kwa amani na mashauriano jumuishi.