Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa OCHA ahimiza kuendelea kutoa misaada na ufumbuzi wa kisiasa Syria

Nembo ya OCHA

Mkuu wa OCHA ahimiza kuendelea kutoa misaada na ufumbuzi wa kisiasa Syria

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, Bi Valerie Amos ameikumbusha jumuiya ya kimataifa kuhusu uzito wa tatizo la kibinadamu la Syria na kusema kuwa, misaada ya ziada inahitajika kabla ya muda mrefu wa majira ya baridi kuanza kwa watu ambao wamefurushwa makwao kufuatia mapigano, na kwa ajili ya nchi zinazowasaidia.

Amos amesema haya katika taarifa baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Uturuki.

Akishukuru Uturuki kwa ukarimu wake wa kuwakaribisha wakimbizi kutoka Syria, Amos amesema, karibu raia 200,000 walikimbilia Ayn Al-Arab Uturuki katika kipindi cha wiki kadhaa na mamlaka za Uturuki ziliwalaki mara moja.

Aidha, Amos ameelezea karibu watu milioni kumi wamekuwa wakimbizi wa ndani au kuondoka Syria kabisa.