Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ya Ebola kuanza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu- WHO

Kirusi cha Ebola:FAO

Chanjo ya Ebola kuanza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu- WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza leo kuwa dawa za chanjo ya Ebola huenda zikaanza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu katika kipindi cha wiki mbili zijazo. Taarifa kamili, na Joshua Mmali.

(Sauti ya Joshua)

Akitoa tangazo hilo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO kuhusu habari na mifumo ya afya, Dr. Marie Paule Kieny, amesema kuna aina mbili za chanjo dhidi ya Ebola, ambazo majaribio yake yataanza wiki mbili zijazo:

“Majaribio haya yataendelea kwa miezi sita hadi mwaka mmoja, lakini kuwa na matokeo ya awali kuhusu usalama wake na kufanya uamuzi kuhusu dozi yake, itakuwa mwishoni mwa mwaka huu, Disemba.”

Majaribio ya chanjo hiyo yatahusisha watu 250 watakaojitolea, wakiwa kati ya umri wa miaka 18 na 65, na wenye afya nzuri. Dr. Kieny ameelezea umuhimu wa majaribio haya

“Majaribio haya yatashirikisha idadi kubwa zaidi ya watu wanaojitolea, na yatakuwa muhimu sana katika kuamua usalama na kinga dhidi ya Ebola, na takwimu hizo zitakuwa muhimu mno katika kufanya uamuzi kuhusu kipimo cha dozi kitakachotumiwa katika kupima ubora wa chanjo hiyo Afrika”

Majaribio yakihitimishwa, chanjo ya Ebola inatarajiwa kuanza kutumiwa Afrika Magharibi mapema mwakani. Haijulikani ni lini chanjo itaanza kutolewa kwa umma kwa ujumla.