Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa sayansi katika amani na maendeleo waangaziwa UM

Mchango wa sayansi katika amani na maendeleo waangaziwa UM

Umoja wa Mataifa leo umeungana na taasisi ya Ulaya kuhusu utafifi wa nyuklia, CERN kuadhimisha miaka 60 ya taasisi hiyo ikiangazia mchango wa Sayansi katika amani na maendeleo. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Shughuli hiyo imehudhuriwa na wanasayansi, watunga sera na hata watendaji wakuu wa Umoja wa mataifa ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ametoa wito kwa wanasayansi kuwekeza kwenye tafiti zitakazochagiza kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya milenia.

Amesema tayari ameuda bodi ya ushauri kuhusu sayansi ili kupanua wigo wa dhima ya sayansi kwenye kazi za Umoja wa Mataifa kwani dunia ya sasa yahitaji sayansi.

(Sauti ya Ban)

“Dunia inakabiliwa na migogoro mingi. Lakini hii pia ni zama zenye fursa, ambapo mafanikio makubwa yawezekana, shukrani kwa sayansi, teknolojia na ubunifu. Kwa wote wanasayansi na watunga sera hapa leo, nawasihi kushirikiana nasi zaidi na kikamilifu katika kujenga dunia yenye amani, ustawi na utu kwa wote.

Rais wa Baraza kuu Sam Kutesa akaweka bayana kuwa sayansi bora ni ile inayobadili maisha ya watu.

(Sauti ya Kutesa)

“Kufika kwa huduma za simu za mkononi na kuhamisha fedha kupitia simu hizo ni moja ya mifano. Sayansi imepanua shughuli za benki, mawasiliano na uwezekano wa kufikia watu majumbani, ikiwa ni pamoja na maeneo yali ndani zaidi."