Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilio cha WFP dhidi ya Ebola chaitikiwa, yapokea dola Milioni 6 kutoka China

Onyo kuhusu athari za ebola mjini Freetown.Agosti 2014.Picha ya FAO

Kilio cha WFP dhidi ya Ebola chaitikiwa, yapokea dola Milioni 6 kutoka China

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limepokea dola Milioni Sita kwa ajili ya kusaidia harakati zake dhidi ya Ebola kwa zaidi ya watu Milioni Moja huko Sierra Leone, Liberia na Guinea.

Msaada huo utagawanywa sawa baina ya nchi hizo tatu, ili kuwezehsa WFP kununua bidhaa muhimu hususan chakula kama vile mchele, dengu na kunde kwa ajili ya mgawo wa dharura kwa watu zaidi ya 300,000 kwa mwezi mmoja.

Mkurugenzi wa WFP Kanda ya Afrika Magharibi, Denise Brown amesema msaada huo umekuja wakati muafaka na hivyo ametoa shukrani kwa China kwani utawezesha kukabiliana pia na utapiamlo miongoni mwa waliokumbwa na Ebola.

Amesema kadri idadi ya wagonjwa inavyozidi kuongezeka, ndivyo WFP itaongeza operesheni yake, japo amesema mojawapo ya changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba wana fedha za kutosha kusaidia wenye mahitaji.