Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumza na wanahabari baada ya ziara Mashariki ya Kati

UN Photo - Jean-Marc Ferre
Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Picha:

Ban azungumza na wanahabari baada ya ziara Mashariki ya Kati

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amewahutubia waandishi wa habari leo mjini New York, baada ya kuerejea kutoka ziara yake Mashariki ya Kati.

Bwana Ban amesema kwenye ziara hiyo aliubeba ujumbe wenye ncha mbili: ukiwa ni kufanya kila juhudi kuikarabati Gaza, na kutopoteza muda ili kuanza tena mazungumzo ya amani.

“Nilikwenda Gaza siku mbili zilizopita kujionea mahitaji mwenyewe. Niliona jamii zilizosambaratika, na uchumi kuharibiwa. Watu wengi mno hawana makazi, na msimu wa baridi unakaribia. Niliondoka gaza na moyo mzito, lakini pia na matumaini. Hali ya Gaza ni dalili ya tatizo kubwa zaidi: mkwamo wa harakati za amani Mashariki ya Kati.”

Mengine aliyogusia Katibu Mkuu ni hali nchini Syria:

“Bado nasikitishwa na hali nchini Syria. Natoa wito hatua zichukuliwe kuzuia mauaji ya halaiki na kuwalinda raia wa Kobane. Lakini tukumbuke kuwa raia kote nchini Syria wamo hatarini.”

Na akamulika pia tatizo la Ebola

“Ebola ni tatizo kubwa na la dharura duniani, ambalo linahitaji kuchukuliwa hatua haraka. Nchi nyingi zimeonyesha mshikamano, lakini tunahitaji kutimiza ahadi zetu. Tunaweza kushinda Ebola, tukishirikiana vyema. Tuna wajibu wa kuchukua hatua.”