Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kunawa mikono ni njia moja ya kupambana na Ebola- UNICEF

Kunawa mkono imetajwa kama jambo muhimu katika kukabiliana na Ebola. Picha ya UNICEF/NYHQ2014-1522/La Rose

Kunawa mikono ni njia moja ya kupambana na Ebola- UNICEF

Shiirika la Kuhudumia watoto, UNICEF, limesema kuwa wakati dunia inapoadhimisha Siku ya Kunawa Mikono, vita dhidi ya kirusi cha Ebola vinaonyesha umuhimu wa kunawa mikono katika kuzuia magonjwa.

Mkuu wa programu za maji na kujisafi katika UNICEF, Sanjay Wijesekera, amesema kuwa kunawa mikono kwa sabuni ni kinga moja iliyo nafuu zaidi na bora zaidi dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na virusi, yakiwemo mafua.

Amesema kuwa wahudumu wa Umoja wa Mataifa Sierra Leone, Liberia na Guinea wanasisitiza umuhimu wa kunawa mikono kama mojawapo ya njia zinazohitajika kukomesha ueneaji wa Ebola.

Mbali na Ebola, takwimu zilizotolewa hivi karibuni na UNICEF na Shirika la Afya Duniani, WHO, zinaonyesha kuwa mnamo mwaka 2013, watoto chini ya umri wa miaka mitano wapatao zaidi ya 340,000, walifariki dunia kutokana na magonjwa ya kuharisha yanayotokana na kukosa maji safi na huduma za kujisafi.